Dk. Philis Nyimbi anayedaiwa kuzaa na Nabii Mwingira.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,
ameingilia kati sakata la Mtume na Nabii Josephat Mwingira kudaiwa kuzaa
na mke wa mtu.
|
JK, aliingilia kati sakata hilo baada ya mume wa mtu, Dk. William T.
Morris, kukamatwa na maofisa wa uhamiaji kisha kutakiwa kufukuzwa nchini
kutokana na kile kinachodaiwa ni ‘shinikizo la mtu mwenye nguvu’.
Habari ambazo Uwazi limezithibitisha ni kwamba baada ya Dk. Morris
kufungua mashtaka akimtuhumu Mwingira kuzaa na mkewe, Dk. Philis Nyimbi,
alikamatwa na maofisa wa uhamiaji kisha kupewa hati ya kutimuliwa
nchini.
Uwazi limebaini kuwa JK ndiye aliyezuia hati hiyo na mpaka sasa, Dk.
Morris, raia wa Liberia, yupo nchini akiendelea na harakati zake za
kusaka haki kisheria kuhusiana na madai yake hayo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
JK ALIMFIKIAJE?
Inaelezwa kuwa wakati Dk. Morris alipokamatwa,
alitokea msamaria mwema (jina tunalo) anayejua ‘njia za kupita’ kufika
Ikulu ambaye alimfikishia JK mkanda mzima wa sakata hilo la Mwingira.
“… (anataja jina la msamaria mwema), alimwambia JK kuwa nchi
inaelekea katika aibu, Dk. Morris ni mtu anayetambulika Umoja wa Mataifa
(UN) hasahasa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
“JK baada ya
kusimuliwa kila kitu, alichokifanya ni kuingilia kati na kuzuia Dk.
Morris asifukuzwe nchini,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
Mtume na Nabii Josephat Mwingira.
“Vilevile JK aliomba namba ya Dk. Morris kisha alimtumia SMS na
baadaye wakaongea, akamhakikishia yupo salama nchini lakini kuhusu madai
yake kuhusu mkewe, aendelee kufuata sheria.”
HATI YAKE BADO INASHIKILIWA NA UHAMIAJI
Habari zaidi zinaweka
kweupe pamoja na JK kuzuia Dk. Morris asitimuliwe nchini, bado maofisa
wa uhamiaji Mkoa wa Pwani, wanashikilia hati yake ya kusafiria
(passport) mpaka leo.
Dk. Morris alipoulizwa kuhusu hilo, alikiri: “Ni kweli wanaishikilia.
Niliwaomba wale maofisa wanipe nyaraka inayoonesha passport yangu
wanaishikilia. Niliogopa wanaweza kunigeuka. Waliniandikia, kwa hiyo
sina wasiwasi.”
Cheti cha ndoa ya Dk. Morris na mkewe Dk. Philis.
SAKATA LENYEWE LIPOJE
Toleo lililopita la gazeti hili, tuliandika habari yenye kichwa Mume: Mwingira amezaa na mke wangu.
Katika habari hiyo, gazeti hili lilisimamia tuhuma zilizofunguliwa na
Dk. Morris kwenye Kituo cha Polisi Kati (Central), Kibaha, Pwani, akidai
Mwingira amezaa na mkewe.
Shauri hilo lilifunguliwa kwa kichwa JALADA LA UCHUNGUZI, nambari KBA/PE/20/2011, mtuhumiwa akiwa Josephat Mwingira.
Habari yetu iliyopita, mke wa Dk. Morris, Dk. Philis, alidai alizaa nje
ya ndoa baada ya kutekelezwa na mumewe, ingawa alikataa kumtaja
mwanaume aliyezaa naye.
Zaidi ya hapo, Dk. Philis alisema Dk. Morris hakuwa mwaminifu kwenye
ndoa, kwani alidiriki kumsaliti kwa binti mwenye umri chini ya miaka 18
ambaye wao kama mke na mume, wangeweza kumzaa.
Mtoto wa Nabii Mwingira aliyezaa na Dk. Philis.
|
DK. MORRIS NA MWANDISHI WETU
Katika kumchimba zaidi Dk. Morris, mwandishi wetu alifanya naye mahojiano kama ifuatavyo;
MWANDISHI: Ni kweli ulimtelekeza mkeo ndiyo maana akaamua kusaliti na kuzaa nje ya ndoa?
DK. MORRIS: Si kweli hata kidogo, amenisingizia, naomba amuogope Mungu.
MWANDISHI: Una ushahidi wowote kuwa ulikuwa unamjali mkeo?
DK. MORRIS: Ushahidi upo wa kutosha. Anazungumzia kipindi cha kuanzia
mwaka 2006 mpaka 2011, ni kipindi ambacho nilikuwa naishi Marekani
kikazi WHO.
Kipindi hicho, nilikuwa namtumia mke wangu dola za
Kimarekani 2500 (zaidi ya shilingi 4,000,000) kila baada ya wiki mbili
lakini kuna wakati nilikuwa nampa zaidi ya hizo.
Gazeti hili lilioneshwa nakala ya karatasi za kibenki zikionesha
jinsi alivyokuwa akimuingizia fedha mkewe aliyekuwa na akaunti katika
Benki ya Standard Chartered Moshi (namba ya akaunti tunaihifadhi), yeye
akiwa Marekani akitumia Bank of America kuanzia mwaka 2006.
MWANDISHI: Hebu niambie, Dk Philis bado ni mke wako? Yeye anasema wewe siyo mumewe.
DK. MORRIS: Ni mke wangu halali wa ndoa takatifu. Nilifunga naye ndoa
katika Kanisa la St Alban, Dar Desemba 23, 2001, nikiwa na umri wa miaka
39 na yeye (mkewe) akiwa na miaka 30.
Ndoa hiyo niliigharamia sana tangu mavazi ya wapambe wangu na wa mke
wangu. Ilikuwa siku ya furaha kabisa. Sikupenda wakwe zangu wapate
shida.
MWANDISHI: Ukiwa Marekani ulipata habari zozote za kuwa mkeo ni mjamzito au kajifungua?
DK. MORRIS: Hapana, sikuwa na habari kabisa juu ya jambo hilo na ndiyo maana nilikuwa nikimtumia fedha za kutosha.
Kuna siku moja aliniambia anataka kwenda kufanya utafiti Afrika Kusini,
akawa anataka dola 2500 siku hiyohiyo aliyoniambia. Nilimwambia
taratibu za fedha Marekani ni ngumu. Nilikwenda ofisini kwangu nikaomba
malipo ya awali ya mshahara wangu, nikamtumia dola za Kimarekani 3,000
(shilingi milioni 4.8 kwa cheji ya sasa).
MWANDISHI: Uliporejea Tanzania, ilikuwaje ukajua mkeo amezaa nje ya ndoa?
DK. MORRIS: Nakumbuka usiku mke wangu alianza kulia. Nilishangaa
nikamuuliza kwa nini unalia, akanijibu kwamba anaomba nimsamehe kwa
sababu amezaa nje ya ndoa.
MWANDISHI: Baada ya kusikia hivyo ulijisikiaje?
DK. MORRIS: Niliishiwa nguvu kabisa, nikamuuliza kwa nini amefanya
usaliti huo? Nilimuuliza ni nani amempa mimba, akaniambia ni mwanaume
mmoja injinia ambaye alidai yupo Marekani kwa wakati huo.
MWANDISHI: Hayo ulikuwa unamuuliza mkiwa wapi Dar au Kibaha?
DK. MORRIS: Tulikuwa Moshi, nikiwa Marekani mke wangu aliniambia yupo
Moshi anachukua shahada ya pili (Master) ya udaktari, na nilikuwa
namtumia fedha za pango la nyumba, lakini pale nilimkuta hotelini, kesho
yake tukarudi Dar.
MWANDISHI: Baada ya kufika Dar mambo yalikuwaje?
DK. MORRIS: Mke wangu aliniambia kuwa ni lazima nimsindikize kwa Nabii
Mwingira ili akaombewe kwa ushetani alioufanya wa kuzaa nje ya ndoa.
MWANDISHI: Ulikubaliana naye?
DK. MORRIS: Nilimkubalia tukaenda
kwa sababu wakati huo nilikuwa sijajua kuwa yeye ndiye mbaya wangu.
Tulimkuta na akatukaribisha ofisini kwake.
MWANDISHI: Mambo yakawaje?
DK. MORRIS: Mwingira alituombea, wakati akituombea Mwingira mwenyewe alilia sana.
MWANDISHI: Ukaja kumtuhumu vipi tena Mwingira kuwa amezaa na mkeo?
DK. MORRIS: Subiri kwanza, kesi ikishakuwa mahakamani yote yatakuwa
wazi. Nitataka pia tupimwe kila kitu, DNA pamoja na Ukimwi.
MWANDISHI: Vipi madai ya wewe kutimuliwa nchini?
DK. MORRIS:
Namshukuru sana Rais Kikwete, ni kiongozi mzuri, alinisaidia sana.
Namuamini, nampenda na nawaomba Watanzania wampende kiongozi huyu, ni
mpenda haki.
MWINGIRA BADO SHIDA
Jitihada za waandishi wetu kumpata Mwingira
bado hazijazaa matunda, kwani kila njia inayotumika, wasaidizi wake
hawataki kabisa kiongozi huyo wa Kanisa la Efatha, afikiwe na kuhojiwa
kuhusu madai haya.
Hata hivyo, Uwazi halijakata tamaa, litaendelea kumsaka mpaka apatikane na kujibu tuhuma hizo