SIKU 4 tangu Rais Jakaya Kikwete alihutubie Bunge na kuweka bayana msimamo wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Kenya imempongeza huku ikisisitiza kuwa nayo itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa na hatua ya
marais, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni (Uganda) na Paul
Kagame wa Rwanda kuanza mazungumzo ya kuitenga Tanzania, lakini akasema
kamwe haitaondoka kwenye jumuiya hiyo.
Alisema nchi hizo zimeanza mazungumzo kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta, jambo linalovunja misingi ya jumuiya hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, jana alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo
ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Membe
alisema Kenya imesema kuwa mazungumzo kati yake na nchi za Uganda na
Rwanda kuhusu ujenzi wa reli na bomba la mafuta yalifanyika bila nchi
yake kujua kwamba inavunja misingi ya jumuiya.
“Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya yuko nchini, ametumwa na rais wake,
Uhuru Kenyatta kuja kutoa pongezi kwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete
aliyoitoa bungeni,” alisema Membe.
Kwa mujibu wa Membe, Kenya ilidai kuwa ilifanya hivyo bila kufahamu
kwamba nchi hizo zinaibagua Tanzania ambayo ni mwanzilishi wa jumuiya
hiyo.
“Tunapongeza hotuba ya Rais Kikwete bungeni na kuahidi kwamba Kenya
itaendelea kuwa mwanachama imara wa jumuiya hiyo, atakayelinda misingi
imara na taratibu zilizowekwa,” alisema Membe akimkariri Waziri wa
Kenya.
Aliongeza kuwa ujumbe huo ulikiri kutokea kwa tatizo hilo, hasa
ikizingatiwa kwamba viongozi wa nchi hiyo wamechukua madaraka Aprili 8,
mwaka huu.
“Kwa ujumla Kenya inasema ilipotoka kufanya mazungumzo kuhusu mambo
ambayo yapo kwenye mkataba bila kuishirikisha Tanzania,” alisema.
Aidha, Mhe. Mohammed alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga
mkono nchi yake katika kesi inayowakabili Rais na Makamu wa Rais wan
chi hiyo huko Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Alieleza
kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono kesi hiyo
iahirishwe hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi
hao kuwatumikia wananchi waliowachagua.
“Tunaishukuru
sana Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Kenya
katika suala linalowakabili viongozi wetu la kushitakiwa
ICC. Tumaamini kabisa kuwa hatuwezi kumaliza kesi hiyo wala kupata
kibali (deferral) cha kesi hiyo kusogezwa mbele bila kuungwa mkono na
nchi kama Tanzania” alisisitiza Mhe. Mohammed.
Awali
akimkaribisha Bibi Mohammed kuzungumza na Waandishi wa Habari, Mhe.
Membe alisema kuwa Serikali ya Tanzania imefurahishwa sana na ziara ya
Ujumbe huo mzito kutoka Kenya na Tanzania inazipokea kwa mikono miwili
pongezi hizo za Kenya kwa Rais Kikwete na kwa Watanzania kwa ujumla.
Kuhusu
suala la viongozi wa Kenya kupelekwa ICC, Mhe. Membe alisema kuwa,
Tanzania bado inaunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na Nchi Wanachama wa
Umoja wa Afrika (AU) ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuahirisha kesi
hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapa nafasi Viongozi hao
kukamilisha baadhi ya mambo waliyojipangia kuyatekeleza kwa nchi yao.
“Tunashukuru
Mwendesha Mashitaka wa ICC ametoa tamko la dharura kwa kesi dhidi ya
Rais Kenyatta kuanza kusikilizwa tarehe 5 Februari, 2014 badala ya
tarehe 12 Desemba, 2013. Hata hivyo bado tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa
kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusogeza mbele kesi hiyo
kwa mwaka mmoja hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa
Viongozi hawa kuitumikia nchi yao kikamilifu kwani tunaamini katika
kipindi hicho Serikali ya Kenya itakamilisha mengi” alisisitiza Mhe. Membe.
Mhe.
Membe aliongeza kuwa, kulingana na kauli ya Mhe. Mohammed alipozungumza
nae, migogoro ya Kenya iliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007
imetatuliwa kwa asilimia 75, ambapo baadhi ya
wahusika wamepatiwa ardhi, watuhumiwa wamepelekwa mahakamani na baadhi
yao wamepewa fidia kutokana na madhara mbalimbali waliyoyapata.
“Tanzania ipo pamoja na Kenya na ipo kuhakikisha Serikali hiyo
inatawalika kwa kuwapa nafasi viongozi waliochaguliwa na wananchi
kuongoza”, alisema Mhe. Membe.
Mkutano
wa pamoja na Waandishi wa Habari kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed
ulifanyika jana katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule na Maafisa Waandamizi kutoka
Serikali zote mbili..
Nchi za Uganda na Rwanda bado hazijasema chochote kuhusiana na hotuba hiyo ya Rais Kikwete.