Majukwaa ya Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba
vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi
mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza
kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo
pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika
mzunguko wa kwanza.
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza
ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa
yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa
CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo
(dressing rooms) havina hadhi).
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea-
pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini
Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya
kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji
mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch
ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi
juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa
viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya
kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya
sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya
utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za
uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya
gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake
kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi
yao, na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya
Ligi.
Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za
washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo
mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa
mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika
tatu.
Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini
ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam.
Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo
atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa
nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa
kupeana mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo
amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.
Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye
benchi la ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la
kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati
ya Maadili.
Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fi
kiri Elias amepigwa faini ya sh.
500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati
wa mechi yao dhidi ya Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo
Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili kwa kumshambulia refa kwa
matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika
FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000
na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti
wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit
Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp
ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo
Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila
mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi
ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile
wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000
na kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa na kutishia
kuhamamisha washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi dhidi
ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa
faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi
kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi
imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT
iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo
haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka
huu).