MTIHANI wa Taifa wa
Kidato cha Nne, umeingia dosari baada ya walimu wawili akiwamo Mkuu wa
Shule, kushikwa wakishiriki kutoa majibu kwa wanafunzi wao. Tayari
Polisi mkoani hapa, inashikilia walimu hao wa Sekondari ya Nkinto
wilayani Mkalama kwa tuhuma ya kuvujisha mtihani huo unaoendelea
kufanyika nchini kote hivi sasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Mkuu wa Shule, Monica Sebastian (30) na msimamizi wa mtihani huo, Agaloslo Otieno (32).
Alisema watuhumiwa hao
walivujisha mtihani huo juzi kati ya saa 3 na 3:30 asubuhi katika shule
hiyo iliyopo Kata ya Mwangeza Tarafa ya Kirumi.
Alidai kuwa Mwalimu
Agaloslo aliyekuwa akisimamia mtihani katika shule nyingine ya Mwangeza,
aliandika baadhi ya maswali ya Kiswahili na Uraia kwenye simu yake ya
mkononi na kumtumia Mkuu wa Shule yake ya Nkinto, Monica aliyekuwa
shuleni kwake.
Baada ya Monica kupata
maswali hayo, inadaiwa alitafuta majibu akiwa chooni huku wanafunzi
wakimfuata huko huko na kupewa majibu.
Kamanda Kamwela alisema
lengo lao lilikuwa kusaidia wanafunzi, wafanye vizuri katika mtihani wao
wa kidato cha nne mwaka huu. Alisema wanafunzi waliishaambiwa
wadanganye wanakwenda chooni, ili wakapewe majibu na Mkuu wa Shule.
"Uchunguzi wa awali
unaonesha kuwa uvujishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya
Monica na Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika shule
tofauti.
“Baada ya Mkuu wa Shule
kutumiwa maswali, alijificha chooni na watahiniwa kwa nyakati tofauti
waliomba ruhusa kwa wasimamizi kwenda kujisaidia na hapo walimkuta Mkuu
wa Shule na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali hayo," alisema
Kamanda Kamwela.
Alisema baada ya Polisi
kupata taarifa ya siri kutoka kwa wasamaria, iliweka mtego katika
Sekondari ya Nkinto na kumkamata Mwalimu Monica huku simu yake ikiwa na
baadhi ya maswali ya mtihani.